Wednesday 8 October 2008

Mbolea ya Mboji katika mjadala


Waalimu wawili wakuu wa shule ya Msingi za Kahama na Kirumba pamoja na Mwalimu toka shule ya msingi Isenga, wakifuatana na Mratibu wa Mradi wa Tampere - Mwanza wametembelea chuo cha TAMK Tampere kujadili maendeleo ya mradi wa utengenezaji wa mbolea katika shule zao jioni ya leo. Pichani Waalimu hao wakitoa maelezo juu ya mradi huo ambao kwa ufupi umekuwa ni wa mafanikio makubwa.

Aidha wanafunzi wa TAMK walipata kutoa shukrani zao juu ya ushirikiano mkubwa wakati wa uanzishaji wa mradi huo wa aina yake wenye lengo la kuwashirikisha wanafunzi katika utengenezaji wa mboji.



Hadi sasa shule zote tano ambazo zipo kwemye mradi huu zimefanikiwa kuzalisha mbolea hiyo, huku shule ya msingi ya Isenga ikiwa tayali imeanza kutumia mbolea hiyo kwa upandaji wa miti katika shule yao. Mwalimu toka Isenga alisema kuwa mafanikio hayo yameanza kuvuka mipaka ya shule hiyo kwa baadhi ya wakaazi wa karibu na shule hiyo kuanza kutengeneza mbolea ya mboji.

Mipango ya baadae ni kuendelea kutoa elimu ya utengenezaji wa mboji kwa shule nyingi zaidi katika Jiji la Mwanza. Aidha kutoa nafasi kwa wanafunzi na wananchi wa jiji hilo kupitia vikundi kazi kutembelea jiji la Tampere ili kutoa ujuzi wao wa kutengeneza mbolea kwa wakaazi wa jiji la Tampere. Hii itakuwa ni nafasi nzuri zaidi kwao, kwani matumizi ya artificial fertilizer yanategemewa kupungua kwa kasi katika nchi ya Finland kutokana na kuongezeka kwa bei yake kwa kiwango cha asilimia 300.

Kwa upande wa TAMK wanafunzi wameonyesha kulidhika sana na mradi huo kiasi kwamba idadi ya wanafunzi wanaotegemewa kwenda kwenye awamu ya pili ya mradi huo imeongezeka. Hii ni changamoto kwa Jiji la Mwanza kuandaa shughuli nyingi kadili ya idadi ya wanafunzi hao ili kuweza kunufaika vema na utaalamu wao.